Haniya Saggar, mke wa marehemu Sheikh Aboud Rogo anakabiliwa na mashtaka matatu mapya ya kukosa kutoa taarifa kwa polisi, kuhusu washukiwa wa ugaidi waliovamia Kituo cha polisi cha Central jijini Mombasa.
Haya yanajiri baada ya Saggar kutiwa mbaroni kwa dhana ya kupokea pesa kutoka kwa mmoja wa washukiwa hao.
Mbugua Murethi, wakili wa Saggar amesema kuwa madai anayohusishwa nayo mteja wake ni ya kusingiziwa, ikizingatiwa kila uchao afisi ya mkuu wa mashtaka ya umma inambadilishia mashtaka.
“Kila siku mteja wangu anabadilishiwa mashtaka. Hii ni wazi kuwa madai haya yote si ya ukweli bali ni njama ya kukandamiza haki za mteja wangu,” alisema Mbugua.
Mbugua ameilaumu afisi ya mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa kwa kutokuwa imara kuhusu madai yanayomkabili Saggar.
Haniya Saggar, Nastaheno Ali Thalili, Luul Ali Thahil na Zamzam Abdi Abdallah wanadaiwa kukosa kutoa habari kwa polisi kuhusu uvamizi wa Kituo cha polisi cha Central.