Mke wa marehemu Sheikh Aboud Rogo anatajariwa kufunguliwa mashtaka leo (Ijumaa) iwapo uchunguzi utathibitisha kuwa yuko na ufahamu wa uvamizi wa Kituo cha polisi cha Central.
Haniya Said Saggar amekaa korokoroni kwa muda wa siku tisa tangu kukamatwa kwake na kuhusishwa na uvamizi wa kituo hicho.
Saagar anatuhumiwa kupokea pesa kutoka kwa mmoja wa washukiwa aliyepigwa risasi baada ya jaribio hilo la shambulizi kutibuka.
Wiki iliyopita, mawakili wake Yusuf Abubakar na Chacha Mwita, waliitaka mahakama kumuachilia huru huku uchunguzi dhidi yake ukiendelea.
Kiongozi wa mashtaka Eugine Wangila alipinga ombi hilo na kuomba muda zaidi wa kufanya uchunguzi .
Wangila alisema kuachiliwa kwa mshukiwa huyo kunaweza kuhujumu uchunguzi wa kesi hiyo.
Saggar alitiwa mbaroni akiwa nyumbani mwake katika eneo la Kanamai, Kaunti ya Kilifi.
Kufikia sasa washukiwa saba wametiwa mbaroni kuhusiana na uvamizi wa kituo hicho cha polisi cha Central.