Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Kopere, Muhoroni katika Kaunti ya Kisumu amewaonya vikali wazazi kukoma kuwatuma wanao ambao ni wanafunzi kuwanunulia pombe na sigara.
Mwalimu huyo mkuu, Suzan Nyaoko ambaye alighadhabishwa sana baada ya kukutana na mwanafunzi mmoja wa shule hiyo akiwa amebeba pombe hivi majuzi, alilaani vikali kitendo hicho na kuonya kuwachukulia hatua kali za kisheria wazazi wanaofanya hivyo, akisema kuwa ni makoksa kumtuma mtoto mdogo wa chini ya umri wa miaka 18 kununua vileo.
“Sitawaacha wazazi kuwapotosha watoto ambao bado wanasoma ambao ni tegemeo la taifa letu kwa siku zijazo. Pombe ni mbaya kwa mtoto na ukianza kumzoesha kuenda kununua ni lazima ataanza kuionja,” alisema mwalimu Nyaoko.
Aidha, Mkuu huyo wa shule amesema kuwa amejaribu kuwaonya wazazi kuwachunga wanao dhidi ya ulevi na kukoma kuwatuma kununua vileo, lakini hawakuchukua hatua zozote, na badala yake wameendelea kuwaelekeza wanao kwenye njia potovu.
Nyaoko sasa anataka Polisi katika eneo hilo kuanzisha msako dhidi ya wagema wa pombe haramu ili kuwanasa na kuwashtaki. Amesema kuwa wagema wengi katika eneo hilo huwauzia watoto walio chini ya umri 18 pombe na kuwasababishia watoto hao kuacha shule mapema kwa sababu za ulevi.
“Wagema hawa wakamatwe na kushtakiwa kufuatia sheria ili iwe funzo kwa wengine na kupunguza visa kama hivyo na ikiwezekana kukomesha tabia hiyo kabisa,” alisema Nyaoko.
Eneo hilo limeshuhudiwa visa vingi ambapo vijana washule hupatikana kwenye vilabu za pombe hata siku za masomo na wengine wao kuvuta sigara hadharani bila kujali.