Mzee mmoja mkongwe ambaye ni mwanafunzi kwenye shule moja ya watu wazima katika eneo la Masogo Wilaya ya Muhoroni katika Kaunti ya Kisumu alisusia darasa kwa siku nzima, akilalamikia mavazi ya mwalimu wake wa kike.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Hillary Akoko mwenye umri wa miaka 74 ambaye alijiunga na shule hiyo ya watu wazima almaarufu, Kumbaru aliamua kukosa somo la mwalimu wake ambaye aliingia darasani akiwa amevalia minisketi fupi.

Duru za kuaminika zinasema kuwa mzee huyo ambaye alionekana kughadhabishwa sana na nguo hiyo fupi, alinyanyuka mara moja na kuondoka nje akiwa mwenye hasira, bila kuomba ruhusa hali ambayo ilimchochea mwalimu huyo kumfuata nje ili kujua kilichomfikia mwanafunzi wake.

“Tafadhali mwalimu naomba uniache pekee yangu na hata ikiwezekana uniruhusu nirudi nyumbani nitakuja kesho. Sitaki kuyaona mavazi uliyovalia kwani naona aibu nyingi sana,” alisema mwanafunzi huyo mkongwe akimjibu mwalimu wake aliyetaka kujua kulikoni.

Gabriel Omolo rafikiye Akoko ambaye pia ni mwanafunzi kwenye darasa moja, alituarifu kuwa mwenzake amekua akilalamikia swala hilo mara kwa mara, na kutishia kuacha masomo iwapo mwalimu huyo hatarekebisha namna ya kuvalia.

“Mwenzangu amelalamika swala hili sana. Hata amemweleza mwalimu mwenyewe mara kwa mara kuwa ataacha shule iwapo hatabadilisha namna ya kuvalia,” alisema Omolo.

Hali hiyo ilisimamisha shughuli za masomo siku nzima wakati mkurugenzi wa shule hiyo, Derick Anyona alipoingilia kati kutafuta suluhu. Anyona alisihi mwalimu huyo kubadili mtindo wake wa kuvaa kwa ajili ya elimu kwa wazee hao, huku akiwataka wanafunzi hao wakongwe pia kuelewa hali ya walimu ambao ni vijana, akisema kuwa wanaenda na wakati.