Mfanyabiashara maarufu ambaye pia ni mkosoaji mkuu wa serikali Jacob Juma ameuawa kwa kupigwa risasi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwa mujibu wa gazeti la The Star, Juma mwenye umri wa miaka 42, alipigwa risasi na watu wasiojulikana karibu na Shule ya Lenana siku ya Alhamisi.

Mkuu wa maafisa wa CID katika eneo la Nairobi Ireri Kamwende alisema mfanyabiashara huyo alikuwa akitoka kwenye baa yake 9.30 usiku alipopigwa risasi na watu waliotoroka kwa pikipiki. Gari hilo lilikuwa na mashimo kumi ya risasi.

Juma amekuwa mkosoaji mkuu wa serikali huku akiwahusisha viongozi wa kuu wa serikali na kashfa za ufisadi kupitia mitandao ya kijamii.

Mfanyabiashara huyo alidai kwamba leseni yake ya kuchimba madini ilipigwa marufuku baada ya kukataa kumhonga aliyekuwa Waziri wa Madini Najib Balala.

Juma pia alidai kuwa fedha za Eurobond zilitumika kuwahonga majaji wa ICC wakati wa kesi iliyokuwa ikiwakabili Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto.