Afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma imepinga kuteuliwa kwa jopo la majaji watatu kusikiliza kesi ya ugaidi inayowakabili wasichana wanne.
Kupitia naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa Alexendra Muteti, aliambia mahakama kuu siku ya Jumanne, kuwa ombi hilo halina msingi wowote wakusikilizwa na majaji watatu.
Hii ni baada ya wakili wa wasichana hao Hamisi Mwadzogo kuwasilisha ombi katika mahakama kuu ya Mombasa kutaka jaji mkuu Willy Mutunga kuteuwa jopo la majaji watatu kusikiliza kesi hiyo kwa kile alichokitaja kuwa afisi ya mkuu wa mashtaka ya umma inaenda kinyume na majukumu yake.
Muteti alimtaka jaji Dora Chepkwonyi kutupilia mbali ombi hilo na kulitaja kukiuka katiba ikizingatiwa kesi hiyo inaweza kusikilizwa na mahakama ya chini.
Wanne hao ni Ummulkheri Sadri Abdalla, Khadija Abubakar, Maryam Said Aboud na Halima Adan wanadaiwa mnamo Marchi 26 mwaka 2015, kufaya mkutano jijini Nairobi, kupanga njama ya kutekeleza shambulizi la kigaidi.
Aidha wanakabiliwa na kesi nyingine, ambapo walishtakiwa kwa kuwa wanachama wa kundi la Al-shabab katika mahakama ya Mombasa.