Mkurugenzi mkuu wa Elimu katika Kaunti ya Kisii Wilfred Chepkawai ametoa onyo kali kwa Shule za Upili ambazo zimezuilia vyeti vya wanafunzi waliofanya mtihani kuwa watachukuliwa hatua za kisheria.
Katika mahojiano na Mwandishi huyu wa Habari siku ya Alhamisi, Chepkawai alizitaka Shule zote za Upili kuwapatia wanafunzi waliofanya mtihani vyeti vyao vya kidato cha nne kama ilivyoamurishwa na Naibu Rais William Ruto mapema mwaka huu.
Chepkawai alisema haya baada ya wanafunzi wengi kutoka Kaunti ya Kisii kulalamikia kunyimwa stakabadhi hizo muhimu na baadhi ya Shule za Upili.
“Nawambia wakuu wa Shule za Upili kuwakabidhi wanafunzi vyeti vyao haraka iwezekanavyo na kama hawatafuata sheria watachukuliwa hatua ya kisheria,” alionya Mkurugenzi Chepkawai.
Chepkawai pia alishangaa kwa nini bado Shule nyingi kutoka Kisii hazitii sheria kutoka kwa Serikali ikizingatiwa kuwa onyo hilo limetolewa mara nyingi na Rais Uhuru Kenyatta pamoja na Naibu wake William Ruto.
Agizo hilo likiwa ni mojawapo ya ahadi ya viongozi hao wawili walipoingia mamlakani kuwa watahakikisha kuwa wanafunzi wote wanapewa stakabadhi zao ili kuendelea na masomo na wengine kuzitumia kutafuta kazi.
"Chochote kinachosemwa na Rais au Naibu wake ni sawa na sheria na sijui kwa nini walimu hawa wawe vizuizi kwa wanafunzi ambao wanataka kujiendeleza kimasomo," alihoji Chepkawai huku akiwataka wanafunzi na hata Waandishi wa Habari kusaidia kuweka orodha ya Shule ambazo zimekaidi amri hiyo ili sheria ichukuliwe dhidi yao.
"Nawaomba wanafunzi husika kuripoti swala hili katika ofisi za wakuu wa Elimu katika maeneo yaliyo karibu nao na ikiwezekana kuweka orodha ya Shule hizo ili zichukuliwe hatua ya kisheria," alisema Chepkawai.