Idara ya Elimu katika Kaunti ya Mombasa imekana madai kwamba kuna shule zilizoongeza kiwango cha karo katika kaunti hiyo.
Idara hiyo ilisema haijapokea malalamishi yoyote kuhusu swala hilo na kwamba haiwezi kudhibitisha madai hayo.
Akiongea na mwandishi huyu siku ya Alhamisi mjini humo, mkurugenzi wa elimu katika kaunti hiyo Abdikadir Kike, alisema kuwa shule za Mombasa zinatoza karo inavyostahili.
“Hatujapokea malalamishi yoyote lakini tunajaribu kufuatilia tuone kama kuna visa vyovyote katika shule za hapa Mombasa ambazo zinaendeleza jambo hilo,” alisema Kike.
Aidha, mkurugenzi huyo amewataka wazazi wenye malalamishi hayo na ambao wameshuhudia hali hiyo kutembelea ofisi za elimu katika kaunti hiyo na kuripoti visa hivyo.
“Kama kuna mzazi ana lawama ya aina yoyote na ana uhakika na kile anachodai, basi yuko huru kutembelea ofisi yoyote ya elimu katika kaunti na ombi lake litasikizwa,” aliongeza Kike.
Kauli ya mkurugenzi huyo inatokana na madai kwamba baadhi ya walimu wakuu nchini wameongeza kiwango cha karo wakati huu muhula wa kwanza unapoanza, huku wazazi katika Kaunti ya Mombasa pia wakilalamikia hali hiyo.