Aliyekuwa waziri wa Ugatuzi, Ann Waiguru aliagiza kampuni moja ya kuandaa mikutano kulipwa sh44 milioni ili kuandaa mkutano ambao haukufanyika.

Share news tips with us here at Hivisasa

Hii ni kufuatia ripoti zilizowasilishwa kwa kamati ya bunge inayochunguza madai ya ubadhirifu wa fedha katika hazina ya vijana siku ya Alhamisi.

Clement Ayungo, ambaye ni mkurugenzi katika hazina ya maendeleo kwa vijana aliiambia kamati ya umma kuhusi uwekezaji PIC kuwa Bruce Odhiambo alimwambia Waiguru alimwagiza ahakikishe pesa zile zimelipwa kwa kampuni ya Saverin Holdings Ltd ilhali hafla ambayo kampuni hiyo ilifaa kuandaa ilikuwa imefutiliwa mbali.

‘‘Odhiambo alinifahamisha kuwa alipokea simu kutoka kwa Waiguru huku akimwagiza alipie hafla ambayo yeye mwenyewe na Waziri huyo walikuwa wameifutilia mbali.’’ alisema Ayungo.

Aidha, ilibainika pia kuwa Waiguru alipuuza wosia kutoka kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi nchini (EACC) wa kuwa aliyekuwa afisa mkuu mtendaji wa hazina ya vijana, Catherini Namuye hafai kuhudumu katika ofisi ya umma.

Namuye na Odhiambo wametajwa kwa pakubwa kuhusika na kupotea kwa sh180 milioni kutoka kwa hazina ya vijana.

Itakumbukwa kwamba siku ya Alhamisi, Waiguru alipinga vikali madai ya yeye kuhusika na ubadhirifu wa pesa katika hazina ya vijana alipofika mbele ya kamati ya bunge kuhusu uwekezaji huku akisisitiza kuwa usemi wa aliyekuwa katibu wa ugatuzi, Peter Mangiti wa kuwa alimfahamisha kuhusu kuwepo kwa ufisadi katika hazina ya viijana na madai ya uwongo.