Mahakama kuu imefutilia mbali agizo la kumtaka mkurugenzi mkuu wa Bandari ya Mombasa Catherine Muturi kufika kizimbani kwa ukiukaji wa agizo la mahakama.
Uamuzi huu unajiri baada ya halmashauri ya bandari nchini (KPA) kuwasilisha ombi la dharura la kutaka kutofikishwa mahakamani kwa mkurugenzi huyo wa KPA, Catherine Muturi mbele ya jaji Mathew Emukule.
Wakili wa halmashauri hiyo Billy Kongore ameiambia mahakama kuwa KPA wanafanya majadiliano na wamiliki wa mabohari hayo ili kesi hiyo kusikilizwa na kuamuliwa nje ya mahakama.
Jaji Emukule amekubali ombi hilo na kuagiza kutofika mahakamani kwa mkurugenzi huyo. Hatua hii inajiri baada ya mahakama kuu kumtaka Catherine kufika mahakamani ili kuweka wazi kwanini alikiuka agizo la mahakama kwa kusimamisha shughuli za mabohari yanayomilikiwa na familia ya gavana wa kaunti ya Mombasa Hassan Joho, licha ya mahakama kuagiza kutofungwa kwa mabohari hayo.
Mabohari ya Portside na Autoports CFSs yalifungwa baada ya kuhusishwa na kuendeleza biashara ghushi. Kesi hiyo itatajwa tena Julai 11 mwaka huu.