Mkurugenzi wa wizara ya elimu katika kaunti ya Nyamira Siloma Kinaiyo amejitokeza kuwaonya vikali watu wanaowabaka wasichana wadogo katika jamii.
Akiwahutubia wanahabari afisini mwake siku ya Jumanne, Kinaiyo alisema kuwa mtu yeyote atakayepatikana na kosa la kuwabaka wasichana wadogo wanaoenda shule atachukuliwa hatua kali za kisheria.
"Visa vya ubakaji wa watoto vimekuwa vikiripotiwa katika maeneo mengi nchini ila kwa wale watu wanaojihuzisha na ubakaji huo, wacha wajue kwamba watakabiliwa kisheria," alisema Kinaiyo.
Kinaiyo aidha aliongeza kwa kuwahimiza wanafunzi hasa wa kike kuepuka kutembea vichorochoroni wakati wa kuenda na kutoka shule ili kuepukana na hali ya kukumbana na watu wenye nia za ubakaji.
"Ningependa kuwashauri wanafunzi hasa wa kike kuepuka maeneo ya vichaka wanapoenda na hata kutoka shule ili kuepukana na uwezekano wa kukutana na watu walio na nia ya kuwabaka wasichana hao," aliongezea Kinaiyo.
Haya yanajiri baada ya mshukiwa mmoja wa ubakaji kutoka eneo la Manga kufikishwa mahakamani kwa kosa la kuwabaka wanafunzi wawili wa shule ya msingi siku chache zilizopita.