Kufuatia agizo la waziri wa elimu nchini Fred Matiang'i kuwataka wakurugenzi wa elimu katika kaunti zote nchini kufanya uchunguzi ili kubaini idadi ya wanafunzi wanaoathirika na funza katika maeneo yao, sasa mkurugenzi wa elimu kaunti ya Nyamira Siloma Kinaiyo amewataka wazazi kuzingatia usafi wa wanao.
Kwenye mahojiano mapema Jumatatu, Kinaiyo aliwataka wazazi kushirikiana na walimu ili kuhakikisha usafi wa hali ya juu unazingatiwa miongoni mwa wanafunzi.
"Hali ya mtu kuathiriwa na funza hutokana na hali ya watu kutozingatia usafi wa mwilini, na ndio maana ninawataka wazazi pamoja na walimu kushirikiana kuhakikisha kuwa wanafunzi wanazingatia usafi wa hali ya juu," alisema Kinaiyo.
Kinaiyo aidha aliongeza kuwa hali ya wanafunzi wengi kuathiriwa na funza husababisha wengi wao kutohudhuria shule, hali inayorudisha nyuma ukuaji wa taifa.
"Ikiwa hatutochukua hatua kuhakikisha kwamba tunakabiliana na janga hili la funza, basi uchumi wa taifa hili utaathirika pakubwa kwa maana wanafunzi wengi watakosa kuhudhuria shule, hali ambayo huenda ikawafanya wanafunzi hao kutochangia ukuaji wa uchumi nchini," aliongezea Kinaiyo.