Mkuu wa Elimu katika Kaunti ya Kisii Charles Nyaribo amewaomba wazazi, walimu na wanafunzi kushirikiana pamoja ili kuinua viwango vya elimu katika Tarafa ya Getembe, katika Kaunti hiyo.
Akiongea katika hafla ya siku kuu ya elimu katika Shule ya Msingi ya Kisii siku ya Alhamisi, Nyaribo amewaomba wazazi kushirikiana na walimu bila kujali ukoo au dini na kukoma kulaumiana kila wakati.
“Kwa matokeo mema ya mtihani, lazima walimu wanafunzi na wazazi washirikiane na kila mmoja kufanya sehemu yake kuhakikisha matokeo bora ya mtihani wa kitaifa,” alisema Nyaribo.
Aidha, aliongeza kuwa shule za umma zitaandikishwa na kupewa vyeti vya kumiliki mashamba yao ili kupunguza visa vya unyakuzi. Alisema jambo hilo linashughulikiwa na Kaunti hiyo kupitia Wizara ya Ardhi.
Tarafa ya Getembe ndiyo ilifanya vyema zaidi katika sehemu za Gusii na Luo Nyanza kwa kuzoa alama wastani ya 283.67 ikilinganishwa na ile ya 283.01 ya mwaka wa 2013. Kufuatia matokeo hayo, walimu wameombwa kuongeza viwango vya elimu ili kujinufaisha kimasomo na haya ni kwa mjibu wa mwaadhili wa Maasai Mara Edward Makori.
Kwingineko, Afisa wa Elimu katika Tarafa hiyo Isaac Nyabayo amesema walimu wanafaa kupewa motisha ili kuendelea kuinua viwango vya elimu katika Kaunti ya Kisii.
Hafla hiyo ilijumuisha shule za umma na zile za kibinafsi huku za kibinafsi zikijizolea zawadi nyingi ikilinganishwa na zile za umma.
Baadhi ya waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Naibu wa Chifu lokesheni ya Kisii ya Kati George Nyamwaka na Daktari Mkuu kutoka Chuo cha Maasai Mara (Kisii) James omari.