Idara ya usalama eneo la Pwani imewatahadharisha viongozi wa kisiasa dhidi ya kutoa matamshi ya uchochezi na chuki, la sivyo watakabiliwa kisheria.
Akitoa onyo hilo mjini Mombasa, Kamanda mkuu wa polisi eneo la Pwani Francis Wanjohi alisema kwamba ukosefu wa ushikamano wa jamii na viongozi wa kisiasa imechangiwa na chuki za kisiasa, na huenda hatua hiyo ikachangia migawanyiko.
Akizungumza mjini Mombasa na wanahabari siku ya Jumatano, Wanjohi alihoji kuwa atakayepatikana akitoa matamshi ya uchochezi na chuki na kuchangia kuwahangaisha wananchi kwa misingi ya kisiasa na ukabila, basi serikali itakabiliana naye kikamilifu.
Amesisitiza kwamba kamwe idara ya polisi haitojali cheo au mamlaka aliyonayo kiongozi ama wananchi katika idara za serikali, uwakilishi wa umma ama uwanasiasa, bali watakuchukuliwa hatua za kisheria kwani huenda ikachangia wakenya kuzozona.
"Tunawaonya viongozi wote, wawe wa kisiasa, kijamii, vijana hata wa kidini kujiepusha na matamshi ya uchochezi na chuki na kudumisha amani kwa sababu hatua hiyo ndiyo inaleta vurugu kwa wananchi," alisema Wanjohi.
Wahati uo huo, afisa huyo amezidi kuwaonya vijana dhidi ya kutumiwa kwa vijana na baadhi ya viongozi walio na malengo ya kuwagawanya wakenya, huku akiwataka kujitenga na watu kama hao na kudumisha amani.
Kamanda huyo mkuu wa polisi ametoa onyo hilo baada ya kushuhudiwa viongozi wa kisiasa wakilumbana hadharani kuhusu sakata ya fedha za mkopo wa dhamana ya Euro.