Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Metamaywa ilioko katika eneo Bunge la Kitutu Masaba Kaunti ya Nyamira ameiomba Serikali ya Kaunti hiyo kuwasaidia katika ujenzi wa vyoo.
Hii ni baada ya Vyoo vilivyo kuwa katika Shule hiyo kuharibiwa na mvua nyingi inayoendelea kunyesha katika eneo hilo.
Akizungumza na Mwandishi huyu wa Habari siku ya Ijumaa, Mkuu huyo Monicah Moraa alisema waliambiwa na Maafisa wa hazina ya CDF ya eneo Bunge la Kitutu Masaba kwamba hamna fedha za kugharamia ujenzi huo na hivyo kuiomba Serikali ya Kaunti kuingilia kati.
Moraa alisema hawakuweza kumfikia Mbunge wa eneo hilo Timothy Bosire licha ya kujaribu kumtafuta hata kwenye simu yake ya rununu.
Alisema itakuwa vigumu kuendelea na masomo wakati ambapo shule zinatarajiwa kufunguliwa mnamo siku ya Jumatatu tarehe nne bila pahali pa kujisaidia iwapo wanafunzi hao watakapohisi kuenda haja ndogo au kubwa.
“Ni bahati nzuri vyoo hivyo vilibomoka wakati wanafunzi hawakuwa wamefungua Shule maanake vingesababisha madhara mengi. Vyoo vyote nane viliharibiwa na mvua,” alisema Moraa akiongeza kuwa anaiomba Serikali ya Kaunti hiyo kupitia kwa Gavana John Nyagarama kuingilia kati na kuwasaidia kwa kuwajengea vyoo ili wanafunzi watakaporejea masomo iwe rahisi.
Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 240 kulingana na Mwalimu Mkuu huyo.