Mlalamishi mmoja katika kesi ya ufisadi inayomkabili mwakilishi wa wadi ya Shanzu Maimuna Salim, amesema anaishi kwa hofu baada ya kutishiwa maisha.
Leah Aketch aliwasilisha ombi la kuondoa kesi hiyo mahakamani baada ya kudai kupokea vitisho.
Aketch aliambia mahakama siku ya Alhamisi kuwa anaofia maisha yake na kusisitiza kuwa ni bora kuondoa kesi hiyo mahakamani.
Ameongeza kuwa alikuwa akipigiwa simu na kupokea jumbe fupi za kutishiwa maisha.
"Nimepokea jumbe na simu nyingi za kunitishia maisha yangu. Wananitaka kuondoa kesi hii mahakamani,” alisema Aketch.
Aidha, alisisitiza kuwa alipiga ripoti katika Kituo cha polisi cha Bamburi na cha Mtwapa lakini hakuna hatua zozote zimechukuliwa.
Hata hivyo, kiongozi wa mashtaka Eugine Wangila amepinga ombi la kutaka kesi hiyo kuondolewa na kutaka mahakama iwape muda wa kuwawezesha kufanya uchunguzi dhidi ya madai hayo ya Aketch.
Wangila pia amesema kuwa tume ya kukabiliana na ufisadi inahusika katika kesi zingine na kuripotiwa kwa visa vya ufisadi dhidi ya tume hiyo ni jambo lilalohitaji uchunguzi zaidi.
Maimuna Salim anadaiwa kupokea hongo ya shilingi milioni 1.5 kutoka kwa Leah Aketch ili kumsaidia kutatua mzozo wa ardhi baina ya yake na serikali ya Kaunti ya Mombasa mnamo Julai, 2015.
Mahakama itatoa umuzi wake Septemba 30, 2016.