Mshukiwa mkuu wa ulanguzi wa pembe za ndovu Feisal Mohammed amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kupatikana na hatia.
Mahakama pia imemuagiza Feisal kulipa faini ya shilingi milioni 20 kwa kosa hilo, huku akitumikia kifungo hicho.
Wakati huo huo, mahakama imewaachilia huru washukiwa wengine wanne waliokuwa wameshtakiwa na Feisal kwa kukosekana ushahidi wa kuwahusisha na kesi hiyo.
Abdul Sadiq, Ghalib Kara, Pravez Mohamed na Abdulmajeed Ibrahim wameondolewa mashtaka hayo.
Akitoa hukumu hiyo siku ya Ijumaa katika makao makuu ya Kenya Marine Park, jijini Mombasa, Hakimu Diana Mochache alisema kuwa ushahidi uliotolewa unamuhusisha pakubwa Feisal na umiliki wa pembe hizo.
“Kulingana na ushahidi uliotolewa, mahakama inamuhukumu Feisal Mohamed kifungo cha miaka 20 na pia faini ya shilingi milioni 20 kwa mshukiwa huyo,” alisema Mochache.
Mnamo Juni mwaka 2014, Feisal alikabiliwa na mashtaka ya ulanguzi wa pembe 314 za ndovu zenye thamani ya shilingi milioni 44 katika eneo la Tudor.
Feisal alitiwa mbaroni mwezi Disemba mwaka 2015 na maafisa wa Interpol nchini Tanzania baada ya kwenda mafichoni.
Kufikia sasa amekaa rumande kwa miezi 18 tangu kutiwa mbaroni.
Wakati huo huo, afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma imetishia kukata rufaa kupinga kuachiliwa huru kwa washukiwa hao wanne.
Naibu mkurungenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa, Alexendra Muteti, alisema atakata rufaa kupinga kuachiliwa huru kwa washukiwa hao, kwa kusema kuwa walifaa kufungwa jela kwa kosa hilo.
Muteti aliongeza kuwa wanne hao walikuwa mstari wa mbele katika kuendeleza biashara hiyo haramu.