Mtu mmoja alijeruhiwa siku ya Jumatatu baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka mjini Nyamira kuelekea mjini Kisii, kuhusika kwenye ajali nje ya Hospitali ya Lamu, mjini Kisii.
Ajali hiyo ilitokea pale ambapo lori la kubeba mchanga lilipoteza mwelekeo na kugonga gari hilo lilokuwa linaelekea katika kituo cha mabasi.
Inaripotiwa kuwa dereva wa gari hilo aina ya Nissan alijaribu kuepa alipoona lori hilo limepoteza mwelekeo lakini juhudi zake ziligonga mwamba na akagongwa huku gari hilo likianguka kwenye mtaro.
Wakizungumza na mwandishi huyu baada ya ajali hiyo, Victor Osanse na Lydia Siro ambao walishuhudia ajali hiyo walisema lori hilo la kubeba mchanga lilikuwa linaondoka kwa steji, dereva aliposhindwa kulidhibiti.
“Gari hilo aina ya Nissan lilikuwa na abiria lakini ni mmoja tu ambaye alijeruhiwa kwa kukatwakatwa na vioo vya madirisha ya gari hilo,” alisema Osanse.
Aliyejeruhiwa alipelekwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii huku dereva na utingo wake wakinusurika majeraha.
Walioshuhudia ajali hiyo wamewataka madereva kuwa makini kila mara wanapokuwa barabarani.