Mmoja wa wezi ambao waliibia nyanya mmoja shilingi laki mbili huko Lari alitiwa nguvuni jana hapo jana na polisi ambao wanasimamia eneo la Rukuma huko Lari.
Ilisemekana kuwa nyanya huyo alikuwa anatoka benki wakati alivamiwa na wezi hao, punde tu baada ya kutoa pesa hizo, na kwa mazungumzo yao walimpumbaza na kumnyanganya pesa hizo.
Waliokuwa karibu walipiga nduru, na kupitia juhudi za polisi, wezi hao walifumaniwa na mmoja aliyetorokea ibada ya mazishi ambayo ilikuwa inafanyika hapo karibu, lakini polisi kwa usaidizi wa raia walimshika.
Mwizi wa pili ambaye alikuwa mwanamke aliweza kutoroka kwa kutumia gari la kifahari ambalo walikuwa nalo aina la Prado, pamoja na pesa za nyanya huyo.
Mwizi aliyeshikwa alifungiwa stesheni ya polisi ya Uplands, Lari, ambako nyanya huyo aliandikisha jinsi aliibiwa na wezi hao.
“Ninasikitika kuona kuwa nyanya amepoteza pesa nyingi hivyo, na naomba polisi wa eneo hili kufanya juu chini ili kupata pesa hizo. Zaidi ni kuwa nawasihi polisi waweke doria zaidi eneo hili ili uhalifu upungue au kuisha kabisa,” alisema Lucy Wambui, mmoja wa wakaaji wa eneo hilo.
Mkuu wa polisi eneo hilo la Lari Alfred Makoma alikemea uhalifu huo na kusema kuwa bado polisi wanasaka mwizi ambaye alitoroka.
“Polisi wamehoji nyanya ambaye alipoteza pesa, na pia tunahoji mwizi ambaye alishikwa kwa matumaini kuwa ujumbe tunaopata utatusaidia kunasa mwizi ambaye alitoroka,” alsiem Makoma.