Seneta wa Mombasa Hassan Omar amesema kuwa viongozi wa Mombasa wanaharibu muda mwingi kuzungumzia maswala ya kibinafsi badala ya mambo yanayowahusu wananchi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Omar alitoa mfano wa mjadala mkubwa unaoendelea kwa sasa kuhusu kuondolewa kwa walinzi wa Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho, ambapo viongozi wengi wamejitokeza kumtetea gavana huyo.

Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Omar alisema wanasiasa wamechukua swala hilo na kulifanya la kisiasa huku wakipuuza mambo muhimu.

“Mambo ya kujadili kwamba walinzi wameondolewa mara bunduki inafaa kurejeshwa yanakera sana wakati kuna huduma muhimu ambazo mwananchi wanakosa,” alisema Omar.

Omar alisema hilo ni swala linalohusu maisha ya mtu binafsi huku akiongeza kuwa walinzi wa Gavana Joho hawana uhusiano wowote na utendakazi wa serikali ya kaunti.

Wakati huo huo, Seneta Omar aliwakosoa viongozi katika serikali ya kaunti hiyo wenye tabia ya kuchukua fursa ya nafasi walizonazo kuonyesha ubabe wao dhidi ya viongozi wengine.

Alisema kuwa katika serikali ya Mombasa kuna baadhi ya viongozi wanaojiweka katika hali ya kwamba wana mamlaka zaidi kuliko wengine.

“Katika uongozi huu wa kaunti, hakuna mtu mdogo wala mtu mkubwa na sote tuko sawa kwa hivyo tuache kupimana,” alisema Omar.

Matamshi ya Seneta Omar yanakuja huku kukiwa na mjadala mkubwa katika eneo hilo wengi wakihoji ikiwa ni sawa kwa Gavana Joho kupokonywa walinzi na pia kuamrishwa kurejesha bunduki kwa serikali.

Baadhi ya viongozi wa upinzani wameanza kujitokeza na kumtetea Gavana Joho wakisema hiyo sio haki na kwamba anadhulumiwa.