Share news tips with us here at Hivisasa

Mwenyekiti wa kamati ya uwekezaji na uhasibu wa pesa za umma PAC Kaunti ya Nyamira, Ezra Mochiemo, amekanusha madai ya kuwadhulumu baadhi ya wafanyikazi wakuu wa serikali ya kaunti.

Hii ni baada ya baadhi ya wafanyikazi hao wa kaunti kumshtumu kwa madai ya kuwadhulumu wafanyikazi wakuu wakati wa mahojiano.

Akihutubia wanahabari afisini mwake siku ya Jumatano, Mochiemo aliyasuta madai hayo nakusema kuwa kamwe kamati yake haitotishika kutekeleza majukumu yake ili kukabiliana na ufisadi.

"Kamati ya PAC ni kamati inayo zingatia uwazi na uwajibikaji kwenye utendakazi wake, hasa tunapo wahoji baadhi ya maafisa kuhusiana na madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka kwa maana sisi huwa na ushahidi. Madai hayo ya mapendeleo na maonevu yanalenga kutuharibia jina," alisema Mochiemo.

Mochiemo alisema kuwa kamwe kamati yake haitotishwa kutekeleza majukumu yake akihoji kuwa tayari kamati hiyo imemwandikia barua katibu wa uajiri kwenye kaunti hiyo Erick Onchana, akiwataka baadhi ya mawaziri kuelezea sababu yakutokuwa na imani na kamati yake.

"Kama kamati hatutishwi kwa lolote kuhusiana na madai ya maonevu kwa baadhi ya maafisa wakuu wa kaunti hii, kwa maana tuna uwezo wakuhoji mtu yeyote bila kujali cheo chake ama mlengo anaoegemea kisiasa. Tayari nimemwandikia barua katibu wa kaunti hii, barua yakuwataka maafisa hao waelezee madai hayo,” alisema Mochiemo.