Seneta wa Kaunti ya Baringo Gideon Moi amezitaka idara mbalimbali za serikali zilizotwikwa majukumu ya kukabiliana na ufisadi kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Moi alisema kuwa hatua hiyo itahakikisha kuwa visa vya ufisadi vinavyoendelea kukithiri nchini vinadhibitiwa.

Akizungumza kwenye kikao na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Moi alisema ni wazi kuwa serikali kuu na zile za kaunti zimegubikwa na ufisadi.

Alisema sharti Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) pamoja na idara nyinginezo za upelelezi zitekeleze majukumu yao kikamilifu ili kuikabili hali hiyo.

“Bila ya idara husika kuwajibikia kikamilifu malengo yao katika kuzuia ubadhirifu wa mali ya umma, Wakenya wataendelea kuzongwa na umaskini na ukosefu wa huduma muhimu serikalini,” alisema Moi.

Kwa upande wake, Seneta wa Kaunti ya Taita Taveta Dan Mwazo alisema swala la ufisadi litasitishwa iwapo Wakenya mashinani watasimama kidete kulipiga vita.

Mwazo alisema swala la ufisadi halipaswi kuingizwa siasa kwa kuwa hali hiyo italemaza vita hivyo na kuufanya ufisadi kuendelea kukita mizizi nchini.