Wafugaji wa mifugo katika eneo bunge la Rongai wametakiwa kuwauza baadhi ya mifugo wao haswa musimu huu wa kiangazi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongea katika eneo bunge lake siku ya Ijumaa, mbunge wa eneo hilo Raymond Moi aliwataka wafugaji kupunguza idadi ya mifugo wao ili kuwaepusha na makali ya njaa wakati huu wa kiangazi.

Alisema kuwa msimu huu wa ukame huenda mifugo wengi wakadhoofika kiafya na hata kufariki,  kutokana na ukosefu wa lishe na maji ya kunywa.

“Msimu wa ukame huenda ukadumu hadi mwezi Aprili na ni vyema tuzuie maafa kwa kuuza baadhi ya mifugo ili wasije wakafariki kwa kukosa maji na chakula,” alisema Moi.

“Hakuna haja ya kuwa na mifugo zaidi ya mia kisha wote wafe koutokana na njaa, ni heri uuze mifugo wengi na ubaki na wachache tu ambao unaweza kuwalisha,” aliongezea Moi.

Moi aliwataka wakulima hao kuweka vyema pesa watakazopata kutokana na mauzo ya mifugo ili wazitumie kuwanunua mifugo wengine wakati mvua zitakaporejea.

“Mkiuza mifugo, ni vyema hizo pesa muziweke katika benki ili wakati msimu wa mvua utakapoingia mzitumie kununua mifugo wengine,” alisema Moi.

Jamii ya Maasai ambao ni wafugaji katika eneo la Rongai kwa miaka mingi wamekumbatia utamaduni wa kufuga mifugo wengi na hata kukaidi ushauri wa kuwauza baadhi ya mifugo wao wakati wa kiangazi.