Share news tips with us here at Hivisasa

Chuo kikuu cha Moi katika bewa kuu Kesses kimepiga marufuku magari ya uchukuzi wa abiria kuingia chuoni humo.

Magari hayo ambayo yanahudumu kati ya mji wa Eldoret na bewa kuu la chuo hicho yamekuwa yakiingia na kupitia chuoni humo kuchukua abiria ambao wengi wao ni wanafunzi.

Idara ya usalama chuoni humo ilisema hatua hiyo ni mojawapo wa mikakati ya chuo kuimarisha usalama wa wanafunzi.

“Tangu tuanze kupokea vitisho vya uvamizi wa kigaidi tumeimarisha juhudi za kuboresha usalama ambapo hatua ya kuzuia matatu kuingia hapa chuoni ni mojawapo wa mikakati hiyo,” alisema afisa mmoja wa usalama chuoni humo.

Afisa huyo ambaye hakutaka jina lake kutajwa alisema kitengo cha usalama kinahisi kuwa wakati mwingine visa vya uhalifu shuleni humo hutekelezwa na watu kutoka nje ya chuo hicho ambao hutumia matatu kuingia chuoni humo ndiposa waliamua kupiga matatu marufuku ndani ya chuo.

Hatua hiyo imeghadhabisha wahudumu wa matatu husika.

Mwenyekiti wa chama cha ushirika cha matatu katika kituo hicho Albert Korir alisema chama hicho kitatumia kila mbinu kupinga mabadiliko hayo kwa msingi kuwa chuo hicho hakikushauriana na wadau wote kabla ya uamuzi huo.

Korir amesema chuo hicho kinatumia kizingizio cha kudorora kwa usalama kunyanyasa wahudumu wa matatu ambapo ameonya kuwa iwapo utawala wa chuo hicho hautabadilisha uamuzi huo wahudumu husika watashiriki maandamano kulalamikia hatua hiyo.

Wakati huo huo chuo hicho kimesema wanafunzi wake wanne ambao walitoweka katika hali tatanishi wanashukiwa kujiunga na makundi ya kigaidi nchini Somalia na Sudan Kusini.

Naibu chansola anayehusika na maswala ya kifedha chuoni humo Profesa David Tuigong alisema uchunguzi wao umebaini kuwa huenda wanafunzi husika wamejiunga na makundi ya kigaidi.