Baada ya tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini kukatalia mbali saini za muungano wa Cord kutaka rasimu ya katiba ifanyiwe marekebisho, sasa mbunge wa Borabu Ben Momanyi amejitokeza kulalamikia vikali hatua hiyo. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kwenye mahojiano kwa njia ya simu siku ya Jumatano, Momanyi alisema kuwa huenda muungano wa kisiasa wa Jubilee ndio uliohujumu mpango wa Cord kutaka katiba ifanyiwe marekebisho.

"Inakuwaje kwamba baadhi ya wanasiasa wa Jubilee akiwemo mbunge wa Garissa mjini Aden Duale na mbunge mteule Johnson Sakaja wanaweza kuwa na ufahamu kwamba saini zetu za kutaka kufanya marekebisho ya katiba sio halali hata kabla ya tume ya IEBC kutangaza hilo wazi, na ndio maana naona kama hii ni njama ya Jubilee," alisema Momanyi. 

Momanyi aidha aliongezea kusema kuwa makamishna wa tume ya IEBC sio waaminifu na wanastahili kuondoka afisini ili wachunguzwe huku akisisitiza kuwa muungano wa Cord utaendelea kuzinikisha katiba kufanyiwa marekebisho. 

"Hata kama tume ya IEBC kwa ushirikiano na Jubilee wanataka kuzima ndoto yetu ya kutaka marekebisho yafanyiwe vipengee fulani vya katiba sisi hatutakufa moyo kuhusiana na hatua hiyo na ndio maana tutafanya kila tuwezalo ili kuhakikisha kuwa marekebisho ya katiba yanafanikiwa na yafaa makamishna wa IEBC waondoke afisini," aliongezea Momanyi.