Mbunge wa eneo la Borabu Ben Momanyi amesema kuwa waziri wa ugatuzi Anne Waiguru sharti atoke afisini kwa muda ili achunguzwe kutokana na madai ya ufisadi unaoikumba wizara yake.
Akihutubu kwenye hafla ya kuchangisha pesa za kuwasaidia kina mama kujiendeleza kwenye uga wa shule ya msingi ya Nyamira siku ya Ijumaa, Momanyi alisema wakati umefika kwa waziri Waiguru kuondoka afisini mara moja ili kupeana nafasi ya kuchunguzwa.
"Haya mambo tunayoyaona kwenye vyombo vya habari kuwa Waiguru ni mfisadi yametuchosha, na tunacho taka kuona sasa ni Waiguru kuondoka afisini kwa haraka ili aruhusu uchunguzi kufanyika," alisema Momanyi.
Mbunge huyo aidha alisema kuwa serikali ya Jubilee imekuwa ikionyesha mapendeleo katika hatua zake za kukabili ufisadi uliokithiri kwenye idara mbalimbali serikalini, huku akimpa changamoto Rais Uhuru kumsimamisha kazi Waiguru ikiwa kweli amejitolea kupambana na ufisadi kwenye serikali yake.
"Inaonekana kwamba kuna wanyama ambao ni wa muhimu kuliko wengine, na ni kama hii serikali ya Jubilee inaonyesha mapendeleo kwenye hatua zake za kukabili ufisadi, na ikiwa kweli rais amejitolea kukabili ufisadi, sharti amsimamishe Waiguru kazi," alisema Momanyi.
Akizungumzia swala la kuunga mkono hoja ya kumwondoa afisini Waiguru, Momanyi alisisitiza kuwa atakuwa kwenye mstari wa mbele wa kuiunga mkono hoja hiyo itakapowasilishwa bungeni mapema wiki kesho na mbunge wa Nandi Alfred Keter.
"Mimi niko tayari kuunga mkono hoja ya mbunge wa Nandi inayomtaka Waiguru kuondoka afisini kwa maana sharti tukabili ufisadi," alisisitiza Momanyi.
Hafla hiyo iliyohudhuriwa na mwakilishi wa kina mama kwenye kaunti ya Nyamira Alice Chae, yule wa kaunti ya Kisii Mary Otara, wa Nandi Zipporah Kering na mwakilishi wa kina mama wa kaunti ya Bomet Cesilia Ngetich ilifanikisha kuchangisha zaidi ya shillingi laki nane.