Serikali ya Kaunti ya Mombasa kwa ushirikiano na serikali kuu itaandaa makala ya saba ya mashindano ya wabunge wa mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza kwenye kikao na waandishi wa habari mjini Mombasa siku ya Jumatano, mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu michezo ya wabunge, Wafula Wamunyinyi, alisema takribani wabunge 1,000 kutoka mataifa wanachama wanatarajiwa kuhudhiria mashindano hayo.

Wamunyinyi ambaye ni mbunge wa eneo bunge la Kanduyi alisema madhumuni ya mashindano hayo ni kuimarisha uwiano na ushirikiano wa uongozi na biashara baina ya mataifa ya Afrika Mashariki.

“Lengo kuu la wabunge wa mataifa ya Afrika Mashariki kuandaa mashindano haya ni kuboresha uhusiano wa kisiasa na kuimarisha urafiki baina ya mataifa wanachama,” alisema Wamunyinyi.

Mashindano hayo yatafanyika mwezi Desemba ambapo wabunge wa mataifa wanachama watashindana katika michezo ya soka, riadha, voliboli na gofu.

Katika makala ya mwaka uliopita iliyoandaliwa mjini Kigali Rwanda, wabunge Wakenya waliibuka mabingwa katika mashindano ya riadha, voliboli na gofu lakini wakapoteza katika fainali ya mchezo wa soka.