Gavana wa Kaunti ya Mombasa Ali Joho ameahidi kulifanya jiji la Mombasa kufikia viwango vya miji mingine ya ulimwengu kwa kuhakikisha kuwa nyumba, upatikanaji wa maji pamoja na miundomsingi inaboreshwa zaidi.
Kwenye hutuba yake wakti wa kufanya uzinduzi rasmi wa ruwaza za 2035 ambayo inalenga kuimarisha jiji hilo siku ya Jumamosi jijini Mombasa, Joho alifafanua kuwa tayari serikali ya Kaunti imeanza na uboreshaji wa miundomsingi na kuimarishwa kwa maeneo ya makazi.
Gavana Joho alisistiza kuwa mradi huo unalenga kubuni kazi kwa wenyeji pamoja na kuwavutia wawekezaji kutoka maeneo mengine ulimwenguni pamoja na kuafikia viwango vya ukuaji wa kiuchumi si tu kwenye kaunti hiyo lakini nchi ya Kenya kwa jumla.
Aidha, kwenye ruwaza hiyo, gavana huyo aliweka wazi kuwa Kaunti ya Mombasa inalenga kuanza mradi muhimu wa kuona kuwa maji ya bahari Hindi yanasafishwa na kutumiwa na wakazi kwa kunywa na vile vile kufaidi miradi mbali mbali ya ukulima na shughuli nyinginezo za nyumnbani.
“Tunataka kuliona jiji la Mombasa likifikia viwango vya miji mingine kwa namna mbali mbali kama vile kuwa na barabara za kisasa, reli za kisasa, pamoja na kuwa na nyumba za kutosha kwa wakazi wa jiji hili,” aliongeza Joho.
Kaunti ya Mombasa imekuwa ya kwanza kuzindua mradi wa kuhakikisha kuwa jiji hilo linakua kwenye sekta zote ili kuvutia uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.
Picha: Picha ya jiji la Mombasa kutoka juu. Gavana wa kaunti hiyo ameahidi kuona jiji hilo kuafikia viwango vya kimataifa kwenye sekta zote na kuboreka zaidi.