Serikali ya Kaunti ya Mombasa imeunda jopo litakaloangazia mchakato wa elimu mashinani, ili kuimarisha viwango vya elimu.
Mkuu wa Idara ya Elimu Kaunti ya Mombasa Tendai Lewa, alisema kuwa jopo hilo litakalosimamia hazina ya elimu katika kaunti hiyo litakuwa na jukumu la kusaka fedha za kuitosheleza sekta ya elimu.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Tendai alisema kuwa jopo hilo litatafuta usaidizi wa kifedha kutoka kwa mashirika na makampuni binafsi ili kuwafadhili wanafunzi wasioweza kumudu gharama ya masomo.
Tendai alisema kuwa kaunti hiyo inahitaji kima cha shilingi bilioni 1.5 kuwakimu wanafunzi wanaohitaji ufadhili wa masomo katika kaunti hiyo.
Aidha, alisema kuwa iwapo jopo lililoteuliwa litafaulu kupata kima cha shilingi laki sita kila mwaka, sekta ya elimu itaimarika.
“Tunahitaji shilingi bilioni 1.5 kuimarisha viwango vya elimu katika kaunti yetu na kuhakikisha kuwa wanafunzi wetu wanapata ufadhili wa kutosha,” alisema Tendai.
Tendai aliwahimiza wadau katika sekta ya elimu kushirikiana ili kuhakikisha kuwa viwango vya elimu vinaimarika.