Katibu mkuu katika Wizara ya uchukuzi na miundo msingi nchini John Mosonik, amesema kwamba kuwepo kwa kashfa za ufisadi katika Shirika la Huduma za feri nchini, ndizo zilizochangia kukithiri kwa tatizo la misongamano katika kivuko cha feri cha Likoni.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatano, Mosonik alisema kwamba amefanya kikao cha mazungumzo na wasimamizi wa shirika hilo na hatua za dharura zitachukuliwa ili kusitisha kuwepo kwa huduma duni.
Mosonik alisema kwamba maafisa wa wizara hiyo watatumwa kuchunguza wa kina huduma za shirika hilo.
Aliwataka walio na habari kuhusu kashfa za ufisadi na dhulma za kimsingi zinazoendelezwa na wasimamizi wa shirika hilo kuwasilisha habari hizo katika wizara hiyo.
"Nimepata habari kuhusu kashfa za ufisadi katika shirika la huduma za feri na nitatuma maafisa wa wizara yangu kuchunguza tuhuma hizo. Hatua za kisheria zitachukuliwa ili kupuguza changamoto hizo,” alisema Mosonik.
Wakati uo huo amewaonya viongozi wa kisiasa pamoja na maafisa wa serikali kukoma kuwachochea wakazi kutokana na kukithiri kwa hitilafu za kimitambo za feri hizo, huku akisema kwamba hatua hiyo huenda ikachangia mafarakano.
Aidha, katibu huyo alisema kwamba serikali imetenga fedha zitakazotumika katika kukarabati feri zilizo na hitilafu za kimitambo ili kupunguza kushuhudiwa kwa misongamano katika kivuko cha Likoni na kuzuia wakazi kukubwa na majeraha wakati wa kuabiri feri hizo.
Hatua ya katibu huyo imejiri baada ya wakazi zaidi ya 11 kujeruhiwa katika mkanyagano uliyoshuhudiwa siku ya Jumatatu katika kivuko cha feri cha Likoni kutokana na feri zilizokuwa zikihudumu kukumbwa na hitilafu za kimitambo.