Moto umeteketezwa bweni la wanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya wasichana ya Kirobon iliyo Rongai kwenye kaunti ya Nakuru na kusababaisha hasara kubwa.
Chanzo cha moto huo uliotokea Jumanne mwendo wa saa kumi na mbili jioni haujabainika.
Hata hivyo, hakuna yeyote aliyejeruhiwa kwa kuwa wanafunzi walikuwa darasani kwa masomo yao ya jioni.
Licha ya hayo, hakuna kitu chochote ambacho kiliweza kuokolewa kutoka kwa bweni hilo .
Kulingana na walioshuhudia moto huo miogoni mwao akiwa mwalimu wa shule hiyo, waligundua moshi ukitoka kutoka kwa mojawapo ya madirisha ya bweni hilo na hapo wakaanza shughuli za uokozi wa mali nyingine ya shule baada ya kuzima umeme.
Wameongeza kuwa moto huo ulisambaa kwa kasi kutokana na matandiko ya wanafunzi.
Ingawa wazima moto wa kaunti ya Nakuru walifika muda mchache baada ya moto huo kuanza, walioshuhudia moto huo wanasema wazima moto hao waliweza tu kuzima jitimoto kadhaa ambavyo vilikuwa vikiendeleza kuteketeza mali iliyokuwa kwenye bweni hilo.
Ni moto ambao uliadhiri takriban wanafunzi mia moja waliokuwa wamefika shuleni kwa masomo ya ziada licha ya kwamba wizara ya elimu imepiga marufuku masomo hayo wakati wa mapumziko.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo hata hivyo alitoweka baada ya wanahabari kutaka maoni kutoka kwake.