Mali ya thamani isiyojulikana imeteketea kwenye bweni moja la shule ya upili ya wavulana ya Nyansabakwa inayopatikana kwenye eneo wadi ya Nyamaiya kaunti ya Nyamira mapema Alhamisi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kulingana na mwalimu mkuu wa shule hiyo Henry Manoti, tayari maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi wa kubaini chanzo cha moto huo uliozuka saa kumi na moja asubuhi na kuteketeza bweni hilo wanakoishi wanafunzi 120.

“Bado hatujabaini chanzo cha moto huu uliozuka majira ya saa kumi na moja asubuhi ila maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi mkali ili kubaini chanzo hasa cha huu mkasa," alisema Manoti.

Manoti aidha aliongeza kwa kuitaka serikali ya kaunti ya Nyamira kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba gari la kuzima moto limenunuliwa ili kusaidia katika hali kama hizi.

“Ingekuwa serikali ya kaunti hii imenunua gari la kuzima moto ingelikuwa rahisi kwetu kukabili visa hivi, na ndio maaa naisihi serikali ya kaunti hii kuhakikisha kuwa gari hilo limenunuliwa," aliongezea Manoti.

Ikumbukwe kwa muda sasa visa vya mikasa ya moto kwenye shule mbalimbali katika kaunti hiyo vimekuwa vikiripotiwa bila hata ya serikali ya kaunti hiyo kuweka mikakati mahususi ya kuvikabili.