Wafanya biashara katika kituo cha kibiashara cha Gwa Kahiga, katika kaunti ndogo ya Subukia, wanakadiria hasara kubwa, baada ya maduka yao ya biashara kuteketea katika mkasa wa moto usiku wa kuamkia leo.
Kulingana na walioshuhudia tukio hilo, moto huo ulianza mwendo wa saa tano, ambapo takriban vyumba kumi ambavyo vinatumika kuendesha bishara mbali mbali, vilishika moto ambao chanzo chake bado hakijajulikana.
John Ngigi ni mmoja wa wafanyaya biashara hao, na inasemekana moto huo ulianza katika duka lake la kuuza nyama na hoteli, huku akisema alifahamishwa na bawabu wa zamu ya usiku katika kituo hicho cha kibiashara kuhusu moto huo.
“Baada ya kupashwa habari za moto katika duka langu, kwa haraka nilifika pahala pa mkasa kisha nikapiga kamsa na kuwaita majirani,” alisema Ngigi.
“Lakini juhudi zetu za kuuzima moto huo na kuokoa mali yetu hazikufua dafu kwani moto huo ulisambaa kwa kasi na upepo mkali ulikuwa ukivuma. Biashara hizi ndizo hutusaidia kupa mkate wa kila siku,” aliongezea Ngigi aliyeonekana mwenye huzuni.
Mmoja wa walio shuhudia tukio hilo, Jane Waweru alisema hawakufanikiwa kuokoa chohote, huku mali hiyo inayokadiriwa kuwa ya maelfu ya pesa ikiteketea hadi kuwa jivu.
Mwakilishi wa eneo hilo Peter Njoroge alipozuru pahala pa mkasa alisema eneo hilo linafaa kuwa na gari ya kuzima moto.
“Serikali ya kaunti inafaa kuleta gari la kuzima moto katika kila kaunti ndogo ili kusaidia kukabiliana na majanga ya moto yanapo tokea,” alisema Njoroge.
Njoroge aliongeza kuwa serikali ya kaunti vile vile inastahili kuanzisha hazina ya dharura ili kuwasaidia waathiriwa wa mikasa ya moto kurejelea maisha yao, jambo lililoungwa mkono na wanabiashara hao.