Mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Nakuru Mary Mbugua amewataka wabunge kutoka kaunti hiyou kumheshimu gavana wa kaunti kama kiongozi aliyechaguliwa kwa wingi wa kura.
Akiongea Alhamisi jioni katika hafla moja mjini Nakuru, Mbugua alisema kuwa gavana Kinuthia Mbugua alichaguliwa kwa wingi wa kura, na itakuwa vyema iwapo wabunge watamheshimu na kumsaidia kutimiza ahadi alizotoa wakati wa kampeini.
Mbugua alisema kuwa inavunja moyo kuona baadhi ya wabunge wakimshambulia gavana kila wakati pasipo sababu maalum.
“Gavana ni kama baba wa boma na hata kama baba amefanya makosa, kuna njia mwafaka ya kumkosoa bila kumkosea heshima,” alisema Mbugua.
“Sisi kama wabunge tunafaa tuwe mstari wa mbele kumsaidia gavana kutekeleza ahadi zake kwa wananchi. Nawaomba wenzangu wakomeshe hii tabia ya kumtupia gavana maneno kila wakati kwani inaonyesha picha mbaya isiyofaa,” alihoji Mbugua.
Mbugua aliongeza kusema kuwa iwapo wabunge watamkosea gavana heshima, basi hata wananchi nao pia watafuata mtindo huo.
“Ni muhimu viongozi watambue kuwa wananchi wanjifunza kutoka kwao na iwapo watakosa adabu basi huenda tabia hiyo ikaigwa na raia,”alisema.
Aliwataka wale wote wasioridhishwa na uongozi wa gavana Mbugua kusubiri hadi mwaka 2017 na wapambane naye katika uchaguzi.
“Uchaguzi utakuja na wapiga kura wataamua kama gavana alifanya kazi au la, kwa hivyo wanaomezea mate kiti cha gavana wasubiri na wampe muda afanye kazi yake,” alimalizia.