Serikali inanuia kuweka kamera za CCTV katika miji ya Mombasa na Nairobi katika siku za hivi karibuni ili kuisaidia kuboresha hali ya usalama.
Akizungumza mjini Nairobi siku ya Jumanne katika hafla ya kuzindua mfumo mpya wa marekebisho katika idara ya polisi, Waziri wa Usalama Joseph Nkaissery alisema hatua hiyo itasaidia idara ya usalama kufuatilia kwa karibu yote yanayofanyika katika miji hiyo, na hivyo kuwawezesha kuwanasa wahalifu.
Aidha, waziri huyo alitoa hakikisho kuwa serikali itaboresha makaazi ya polisi nchini kwa kuwajengea nyumba mpya.
“Kila afisa ataweza kuishi kwa nyumba yake tofauti kinyume na sasa ambapo wengine wanalazimika kutumia chumba kimoja,” alisema Nkaissery.
Nkaissery aidha alipinga madai kuwa idara ya polisi ndiyo inaongoza kwa ufisadi nchini kwa kusema kuwa idara hiyo humulikwa tu kwa mabaya badala ya kuangaziwa huduma inazotoa kwa wananchi.
Kulingana na Nkaissery, asilimia nne pekee ya maafisa wa polisi ndio wanaoshiriki ufisadi.