Mke wa gavana wa Kaunti ya Nyamira, Naumi Nyagarama na mawaziri wa kaunti hiyo wameanzisha mradi wa kusafisha miji katika kaunti hiyo.
Mradi huo wa kusafisha miji kwa jina ‘Mradi Safisha Mji’ ulianzishwa siku ya Jumanne katika soko la Kebirigo.
Naumi alisema wataendelea kusafisha miji mingine ili kuhakikisha kaunti hiyo iko na mazingira ya kupendeza.
“Tumekuja kama serikali ya kaunti kusafisha miji katika kaunti hii. Tutaanzia hapa Kebirigo tuende Nyamira town, Ikonge, Keroka, Magombo na Miruka ili mazingira yawe masafi katika kaunti yetu,” alisema Naumi Nyagarama.
Aliongezea: “Tutahakikisha kuwa kwa majuma mawili yajayo, haya maji machafu ambayo hupitia hapa katika soko la Kebirigo yanapitia kwa mifereji maana mabomba yameanza kuwekwa leo. Tunahitaji kaunti hii iwe safi ili wanabiashara wafanyie biashara zao mahala palipo pasafi,” aliongeza Naumi Nyagarama.
Mke wa Nyagarama aliandamana na mwakilishi wa wadi ya Kebirigo Robinson Mocheche ,Mwakilishi wa wadi ya Nyamira Township Robert Ongwano kwa usafishaji huo wa miji katika kaunti hiyo.
“Hii ni njia mojawapo ya kutunza mazingira na hata kuvutia wanunuzi katika soko zetu. Wananuzi watakuja kwa wingi kwa maana wengi wao hupenda kununua bidhaa mahala pasafi. Biashara ikinawiri, tutakua tumefukuza umaskini katika eneo hili,”alisema Robnson Mocheche.