Share news tips with us here at Hivisasa

Wakaazi wa Kaunti ya Lamu wamewakashifu vikali baadhi ya viongozi wa kaunti hiyo wanaounga mkono hatua ya kutengwa kwa ardhi ya hekari elfu 28 katika kaunti hiyo.

Ardhi hiyo inayotengwa ili kutumika kwa mradi wa ujenzi wa bandari mpya ya Lamu (Lamu Port-Southern Sudan-Ethiopa Transport Corridor)LAPSSET wakisema kuwa mradi huo unalenga kuwakandamiza.

Makundi ya akina Mama, Vijana na Wanaharakati wa kisiasa wamewakashifu Seneta wa Kaunti hiyo Abu Chiaba, Mwakilishi wa Kike Shakilah Abdallah na Mbunge wa Lamu Magharibi Julius Ndegwa kwa kusema kuwa Wakaazi hao tayari walilipwa fidiwa.

Mwanaharakati wa kisiasa eneo hilo Mohammed Salim amesema kuwa Viongozi hao watatu wanadaiwa kusema kuwa wakaazi hao wanapaswa kuondoka ili kutoa nafasi kwa mradi huo, kutokana na kuwa tayari walifidiwa. 

lakini kulingana na Salim waliyofidiwa ni wakaazi wa Kilelana pekee na wala sio waathiriwa wote hivyo basi wakaazi hao hawatahama ardhi zao.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu alipoitisha kikao na wanahabari, Salim amesema kuwa iwapo mradi huo utatekelezwa basi zaidi ya familia elfu tatu zitaathirika huku akiahidi kutokubali ardhi hiyo kuchukuliwa pasipo na mpangilio wowote wa kufidiwa wala kuwatafutia ardhi mbadala.

"Sisi kama wakaazi wa kaunti ya Lamu hatutakubali kudhulumiwa tukiona kwa sababu ardhi ni yetu na iwapo tutalazimishwa kuondoka tutaelekea wapi na hatujapewa mahali mbadala pakuishi," alisema Salim.

"Tume ya kitaifa ya ardhi inafaa kueleza bayana swala hili na wala sio kuwashinikiza wakaazi kuhama ardhi yao bila mpangilio wowote kuafikiwa," aliongeza Salim.