Wakaazi wa Kaunti ya Nyamira na Kisii wana kila sababu ya kutabasamu baada ya Waziri wa Maji nchini, Judy Wakungu, kuanzisha  uchimbaji wa kisima cha maji masafi ambacho kitawasaidia wakaazi wa kaunti hizo mbili.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza siku ya Jumatatu katika wadi ya Gesima, iliyoko kaunti ya Nyamira, ambapo kisima hicho kitachimbwa, waziri huyo alisema kuwa serikali ya kitaifa itatumia shillingi millioni 366 kwa uchimbaji wa kisima hicho ambacho kilianzishwa jana katika eneo la Gesima.

Maji hayo yatawasaidia wakaazi zaidi ya elfu 60 wa kaunti ya Nyamira pamoja na ya Kisii. Wakaazi walifurahishwa na mradi huo kwani maji yamekuwa shida kwa wakaazi hao.

“Tumeanzisha mradi wa maji hapa Gesima na hatutaki wakaazi wa eneo la Kisii muwe na shida ya maji maana tayari tumeanzisha kisima hicho cha maji ambacho kitasaidia kaunti hizi mbili,” alisema Wakungu.

Wakati huo huo, waziri huyo alishukuru benki ya Africa Development kwa msaada benki hiyo uliotoa wa shilllingi billion 1.3 za kusaidia uchimbaji wa maji kote nchini.

“Nataka kushukuru benki ya Africa development kwa kuona wananchi wa Kenya wako na shida ya maji na kukabidhi wizara ya maji pesa taslimu ya shilllingi billion 1.3 ambazo zitasaidia uchimbaji wa maji kote chini. Watu watakuwa na furaha kwa maji jambo ambalo limeonekana kuwa changamoto hapa nchini kwa wananchi,”aliongezea Wakungu.

Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama alishukuru mradi huo wa maji na kusema kuwa mradi huo utasaidia wananchi na kupunguza shida ya maji kwa wakazi wa Nyamira na Kisii.