Serikali ya kaunti ya Mombasa imeshikilia kuwa mradi wa uboreshaji wa mji wa Mombasa kwa kubomoa na kujenga upya makaazi ya wakaazi wanaoishi katika nyumba kuu kuu utaendelea licha ya baadhi ya viongozi kupinga mradi huo.
Waziri wa ardhi, makao na mipangilio ya mji kaunti ya Mombasa Antony Njaramba, amesema kuwa mradi huo lazima utatekelezwa licha ya viongozi kuupinga kwani tayari shilingi bilioni 200 za mradi huo zimetengwa.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, Njaramba amesema kuwa iwapo wakaazi wanahisi kuwa wanakandamizwa na serikali ya kaunti hiyo basi wanahaki kufuki mbele ya viongozi wa kaunti hiyo na kujadiliana kwa kina badala ya kuwahusisha viongozi wa kisiasa na kusababisha chuki miongoni mwa wakaazi.
"Tungependa kuwaambia wakaazi iwapo wako na wasiwasi kuhusu mradi huo basi wafike kwetu tuzungumza nao vizuri tuwaeleze vile watafaidika na mradi huo baada ya kukamilika kujengwa," alieleza Njaramba.
Waziri huyo wa ardhi kaunti ya Mombasa amesema kuwa tayari mipango ya kuanza shughuli hiyo na mkataba na wawekezaji wa mradi huo unaelekea kukamilika huku akisema kuwa kamwe kaunti ya Mombasa haitatikishwa na wapinzani dhdi ya mradi huo.