Kaunti ya nyamira imefaidi na mradi wa kujengewa mahakama kuu kuanzia bajeti ya mwaka na kukamilika mwisho wa mwezi wa sita mwaka ujao wa 2016.
Akiongea siku ya Ijumaa na waandishi wa habari katika mji wa Nyamira, mshirikishi wa mpango wa ujenzi sura mpya za mahakama hapa nchini Nancy Kanyako aliwahakikishia wakaazi wa kaunti hiyo kuwa watajengewa mahakama kuu na kuacha kuenda hadi kaunti ya Kisii kushughulikiwa kesi zao ambazo zimekuwa zikileta msongamano kwenye kaunti hiyo.
“Kuanzia mwaka ujao, hamtakuwa na mnahangaika kuenda katika kaunti ya Kisii kwa kusikilizwa kwa kesi zenu, kuwa na moyo wa subira sasa ni rasmi kuwa ujenzi wa mahakama kuu ya hapa kaunti ya Nyamira utaanza hivi karibuni”
Mradi huo ulianza mwaka jana na unafadhiliwa na Benki Kuu ya Ulimwengu kwa ushirikiano na serikali ya Kenya, na ni harakati mojawapo ya serikali ya Jubilee kuleta huduma karibu na wananchi.
Kwa upande wake, hakimu mkuu wa Mahakama ya Nyamira Walter Onchuru alishukuru wahusika wa mradi huo na kusema kuwa utekelezwaji na ujenzi huo utawarahisishia wakaazi wa kaunti ya Nyamira walio na kesi nyingi kwenye mahamaka kuu ya Kisii.
“Mradi huu utatufaidi wote kama jamii na wakaazi wote wote ambao wamekuwa na kesi huku kaunti ya Kisii, watakuwa na huduma hapa karibu kufika katikati ya mwaka ujao na nawaomba wote muwe na subira mambo yatakuwa mazuri hivi karibuni,” alisema hakimu.
Mradi huo unatarajia kugharimu zaidi ya shilingi milioni 120 kukamilika.