Chama cha Jubilee tawi la Mombasa kimezindua mradi wa Vijana na Jubilee unaolenga kuwaunganisha vijana kutoka kaunti za kanda ya Pwani.
Uzinduzi huo ambao ulifanyika katika ukumbi wa Mombasa Women uliwaleta pamoja vijana kutoka Kaunti ya Mombasa, ili kuwarai kujiunga na chama hicho kipya cha Jubilee.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, mwenyekiti wa Jubilee kanda ya Pwani Abdulrahman Mahmud, alisema lengo lao ni kuhakikisha vijana kutoka Pwani wanapata ajira ili kujiepusha na janga la mihadarati ambalo limekuwa donda sugu katika eneo hilo.
Aidha, Mahmud aliwasihi vijana wa kanda hiyo kujiunga na chama cha Jubilee, alichokitaja kama chama cha kipekee kitakachotatua matatizo yanayowakumba vijana wa eneo hilo.
Wakati huo huo, mwenyekiti wa kitaifa wa mradi wa Vijana na Jubilee James Wanjohi alisema mbali na Mombasa, mradi huo umezinduliwa katika kaunti zote 47 nchini.
Alisema kuwa vijana wameweza kufaidika na serikali ya Jubilee kutokana na miradi kama vile Uwezo Fund na Tume ya huduma kwa vijana NYS.