Mratibu wa wakimbizi nchini Keffah Magenyi ameitaka serikali kuu kusuluhisha swala la wakimbizi hisaniwa ili kuzuia migogoro inayoshuhudiwa kila kuchao.
Akiongea Ijumaa mjini Nakuru, Magenyi anayeongoza muungano wa wakimbizi nchini maarufu National IDPS Network, amesema kuwa swala la wakimbizi limechangia pakubwa katika kuzuilia maendeleo katika taifa la Kenya
"Ningependa serikali iwachunguze na kuwachukulia hatua walaghai wanaofuja pesa za wananchi wasio na ufahamu kwa kuwadanganya kuwahusisha katika orodha ya watakaofidiwa," Magenyi alisema.
Kwa mujibu wao ni kuwa jumla ya wakimbizi 11,000 tayari wamepewa makao wakihoji hamna wakimbizi waliosalia kwenye kampi ila wakimbizi hisaniwa.
Wameweka bayana kuwa wameanza zoezi ya kuweka rekodi familia zilizowasitiri wakimbizi hao ili kupata taarifa mwafaka kuhusu wakimbizi hao.
Haya yamejiri huku rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto mwishoni mwa mwezi jana wakati wa hafla ya maombi mjini Nakuru, wakiahidi kutoa suluhu la kudumu kwa wakimbizi hao .