Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Vuguvugu la MRC lililogonga vichwa vya habari miaka ya hivi karibuni kutokana na harakati zake katika eneo la Pwani, huku likiendela kupata upinzani mkali kutoka kwa wanasiasa wa eneo hilo, baadhi yao wakilikashifu hadharani.

Vuguvugu hilo lilituhumiwa na serikali kwa kuendeleza harakati za kuwashawishi wakaazi kuunga mkono wazo la eneo hilo kujitenga kama taifa huru.

Akizungumza siku ya Jumanne, Mbunge wa Matuga Hassan Mwanyoha alitaja kundi hilo kama lililopitwa na wakati na kuwasihi wananchi kujihusisha zaidi na maswala ya maendeleo.

“MRC sio kitu cha kuzingatia kwa sasa. Kitu muhimu kwa wananchi ni kushikana pamoja na viongozi tuliowachagua ili kuleta maendeleo,” alisema Mwanyoha.

Hapo awali, idara ya usalama ilidai kuwa kundi hilo linawashawishi wakaazi kususia zoezi la kujisajili kuchukua vitambulisho vya kitaifa.

Hatua hiyo ilipelekea idadi kubwa ya wanachama hao kukamatwa na kufunguliwa mashataka gerezani ikiwa ni pamoja na kiongozi wa kundi hilo Omar Mwamnuadzi.

Hata hivyo, mbunge huyo kwa sasa amewasihi Wapwani kuchangamkia zoezi la kujiandikisha kama wapiga kura huku akiongeza kuwa kundi hilo sio tishio tena kama ilivyodhaniwa.

“Tuhakikishe kwamba kila kitu kinazungumziwa katika mabunge yetu kwa sababu tuko huru sasa,” aliongeza mbunge huyo.