Msemaji wa vuguvugu la MRC Mohammed Mraja (kushoto) katika hafla ya awali. [Picha/ voanews.com]
Baraza la MRC limekanusha madai kwamba litakata vidole vya watu ambao watapiga kura siku ya Alhamisi.Haya yanajiri baada ya kuibuka porojo kwamba wanachama wa MRC wanapanga kutembea kila nyumba na kuwakata vidole watakaoshiriki katika marudio ya kura za urais.Aidha, baraza hilo limekanusha madai ya kuhusika na karatasi zinazosambazwa za kuwaonya Wapwani dhidi ya kushiriki zoezi hilo.Kwenye kikao na wanahabari siku ya Jumatano, msemaji wa MRC Mohammed Mraja, ameyataja madai hayo kama yanayonuia kuliharibia jina vuguvugu hilo.“Hii ni njama ya kuchafulia jina kundi la MRC, wanaoeneza uvumi huo wanataka tutiwe mbaroni na polisi,” alisema Mraja.Mraja amewataka Wapwani kutoamini propaganda hizo na kuwasihi wale ambao watashiriki zoezi hilo kutohofia usalama wao.Aidha, Mraja amewataka wale ambao hawatashiriki zoezi hilo kutozua fujo kwa nia ya kuvuruga uchaguzi wa kesho.Vile vile, ameitaka idara ya usalama kuwachukulia hatua wale wanaoeneza porojo hizo.“Sharti maafisa wa usalama wawatie mbaroni wanaoeneza madai hayo dhidi yetu,” alisema Mraja.Wakati huo huo, wanachama wa vuguvugu hilo wameweka wazi kwamba hawapingi kufanyika kwa marudio ya uchaguzi nchini na kusisitiza kwamba hiyo ni haki ya kila Mkenya.Huku hayo yakijiri, Kamishna wa Tume ya uwiano na utengamano Irene Wanyoike, amelitaja kundi la MRC kama kundi linalofuata sheria, hivyo basi kulitenga na porojo zinazoenezwa dhidi yake.“Kwa muda sasa MRC imekuwa mstari wa mbele kueneza amani na wala kundi hilo halijasambaza porojo hizo kamwe,” alisema Wanyoieke.Wanyoike ameitaka idara ya usalama kuwatia mbaroni wanaosambaza porojo hizo ili wakabiliwe kisheria.“Maafisa wa usalama wanapaswa kufanya uchunguzi na kuwatia mbaroni wanaotaka kuvuruga amani Pwani,” alisema Wanyoike.