Safari ya kikundi kimoja cha wanawake kuelekea katika hafla ya kanisa jijini Nairobi, Ijumaa iligeuka na kuwa kilio baada ya mmoja wao kuzirai na kuaga dunia mjini Naivasha katika hali tatanishi.
Akina mama hao kutoka Magharibi mwa Kenya walikuwa wakielekea jijini Nairobi wakati mwendazake alizirai katika eneo la Delaramere yapata kilomita mbili kutoka mji wa Naivasha.
Mmoja wa akina mama hao aliyeomba jina lake kubanwa alisema: "Mimi sikuona kama alikuwa na ugonjwa wowote, lakini alisema tusimame hapa Delamere ili ajisaidie, lakini akaanguka ndani ya basi, na kuaga dunia papo hapo".
Afisa msimamizi wa hospitali kuu ya wilaya ya Naivasha Dkt Joseph Mburu alisema kuwa mwanamke huyo alidhibitishwa kuaga dunia alipofikishwa katika hospitali hiyo.
Habari za kuaminika zimearifu mwandishi huyu kuwa mwanamke huyo ni jamaa wa karibu wa afisa mmoja wa ngazi ya juu katika idara ya polisi nchini.
Polisi wa kituo cha Naivasha waliuchukua mwili huo na kuupeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali kuu ya wilaya hiyo.