Mkuu wa polisi eneo la Likoni amesema kuwa maafisa wa polisi wataendeleza msako dhidi ya bodaboda ambazo hazijasajiliwa, kama njia moja ya kukabiliana na visa vya uhalifu.
Willy Simba amesema hatua hiyo imeafikiwa baada ya idara ya ujasusi kupata taarifa kwamba baadhi ya pikipiki ambazo hazijasajiliwa hutumika kutekeleza visa vya wizi.
Akizungumza na wanahabari katika kituo cha polisi cha Likoni baada ya kufanya msako siku ya Jumanne, Simba alisema watahakikisha zoezi hilo linafanikiwa licha ya wahudumu hao kupinga hatua hiyo.
“Huu msako utaendelea kila mahali na lazima watu wafuate sheria. Idara ya ujasusi imegundua kuwa majambazi wanatumia pikipiki kufanya uhalifu hapa Likoni,” alisema Simba.
Kauli ya mkuu huyo wa polisi inajiri huku visa zaidi ya vitatu vikiripotiwa kwa muda usiopungua mwezi mmoja, ambapo wahalifu hao wameonekana kulenga zaidi biashara za M-Pesa.
Simba alisisitiza kuwa zoezi hilo litaendelea licha ya wahudumu wa bodaboda kuvamia kituo hicho siku ya Jumanne, wakitaka wenzao waliokanaswa kuachiliwa huru.
Wahudumu 20 wa bodaboda na wengine wanane wa tuktuk tayari wamekatwa na kuzuiliwa kituoni humo kwa makosa ya kuendesha biashara bila vibali rasmi.