Idara ya usalama katika kaunti ya Uasin Gishu imeanzisha msako dhidi ya genge la majambazi ambao wamekuwa wakiwahaingaisha wakazi wa mitaa ya mabanda mjini Eldoret.
Idara ya usalama mjini humo ilisema kuwa genge hilo la watu zaidi ya 20 limekuwa likiwahangaisha wakazi kwa zaidi ya miezi sita zilizopita.
Akizungumza afisi mwake siku ya Alhamisi, Kamishna wa Kaunti ya Uasin Gishu Bw Abdi Hassan alisema idara ya usalama imepata taarifa muhimu, ambayo itawawezesha kutia mbaroni washukiwa hao.
Bw Hassan alisema genge hilo huendesha shughuli zake katika mitaa ya Langas, Munyaka, Huruma, Kamukunji miongoni mwa maeneo mengine.
“Tumepata habari muhimu kuhusu kundi la majambazi ambao wamekuwa wakiwahangaisha wananchi na kwa sasa tunaendeleza msako dhidi ya genge hilo,” alisema Hassan.
Hasssan alisema mbali na kusaka genge hilo, marufuku ya usafiri wa pikipiki za uchukuzi wa abiria al maarufu bodaboda baada ya saa tano usiku ingalipo.
“Bado tumepiga marufuku wahudumu wa bodaboda kusafirisha abiria baada ya saa tano usiku hadi saa kumi na moja asubuhi. Wahudumu hao ndio husafirisha majambazi usiku,” alisema Hassan.
Wakati huo huo Bw Hassan ametaka vitengo vya usalama mjini Eldoret kushirikiana na viongozi wa Nyumba Kumi ili kumaliza uhalifu katika mitaa mbalimbali mjini humo.
Kulingana na Hassan, kuna mipango ya kufanyia marekebisho mpango wa Nyumba Kumi na kubuni sera ambayo itaboresha utendajikazi wa mpango huo.