Wakaazi wa Mtaa wa Nyamasaria mjini Kisumu wanayo kila sababu ya kutabasamu kwa kupata Msamaria mwenye moyo wa ukarimu na huruma ambaye anawafaa kwa dhiki.

Share news tips with us here at Hivisasa

Tom Otieno ambaye ni mfanyibiashara pamoja na mkulima kwenye eneo hilo amejitolea kusaidia kubeba mizigo ya wakaazi kwa kuwapa msaada wake kwa njia nyingi, akiwa na nia ya kuinua watu wa chini katika jamii kutoka eneo hilo.

Mnamo mwaka uliopita, Otieno alianza kutoa msaada wa masomo, mavazi na lishe kwa jamii ya eneo hilo akionyesha upendo wa kipekee kwa wajane na mayatima.

Msamaria Otieno anatoa pesa zake kuwalipia karo wanafunzi kutoka katika jamii zisizojiweza na vile vile kuwanunulia mavazi na vyakula pamoja na kushughulikia afya yao.

Anasema kuwa anafanya hayo kwa roho safi bila misingi ya kujinufaisha, wala kutaka umaarufu kutokana na matendo hayo mema.

“Niliguswa na moyo wa huruma kutokana na hali ya ufukara ambayo inaendelea katika eneo hili inayolenga kusambaratisha maisha ya wengi,” alisema Otieno.

Aliongeza kuwa, “Baadhi ya wanafunzi ambao nawalipia karo shuleni ukitazama wazazi wao ni wale walala hoi ambao hawawezi kumudu elimu ya wanao.”

Msamaria Otieno ana idadi ya watoto wanane ambao anawalipia karo, sita kwenye shule ya msingi na wawili wakiwa kwenye shule ya upili.

Aidha, Otieno anatoa wito kwa wengine zaidi kujitokeza katika jamii hiyo ili kusaidiana kupunguza hali ngumu ya maisha miongoni mwao, akisema kuwa kutoa na kusaidia ni moyo na wala sio utajiri.