Mshauri wa kifedha wa benki ya dunia tawi la Kenya Charles Mochama amejitokeza kuishtumu vikali serikali ya kaunti ya Nyamira kwa usimamizi mbaya wa raslimali za umma.
Kwenye mahojiano kwa njia ya simu siku ya Ijumaa, Mochama alisema kuwa serikali ya kaunti ya Nyamira imekuwa ikiwekeza raslimali kwenye miradi isiyo na umuhimu.
"Usimamizi na matumizi ya raslimali za umma katika kaunti ya Nyamira ndiyo changamoto kubwa inayoikumba serikali hiyo kwa maana kuna miradi isiyo na umuhimu na ambayo hupewa ufadhili," alisema Mochama.
Mochama aidha aliishtumu vikali serikali ya kaunti hiyo kwa mapendeleo kwenye uajiri wa wafanyakazi wa serikali huku akiongeza kwa kuwarahi wananchi kutopiga kura kwa misingi ya kiukoo.
"Serikali ya kaunti ya Nyamira imekuwa ikiwaajiri wafanyakazi wake kwa njia ya mapendeleo na kiukoo na ni ombi langu kwa wananchi kutopiga kura kwa misingi ya kiukoo kwenye uchaguzi mkuu ujao," aliongezea Mochama.