Mahakama ya Nakuru imemwachilia kwa dhamana ya shilingi 700,000 mwanamme wa makamo ambaye alishtakiwa kwa kosa la kuchapisha jumbe zenye vitisho vya kigaidi kwenye mtandao.

Share news tips with us here at Hivisasa

Hakimu wa Nakuru Felix Kombo pia amemzuia mshatakiwa Robert Mungai, kwa jina lingine Robert Mohamed Bluez kusafiri kutoka kaunti ya Nakuru.

Pia Kombo alimwagiza Mungai kuripoti kwa afisi za upelelezi mara moja kwa wiki.

Mungai alishtakiwa kwa kuchapisha kwenye mtandao wake wa kijamii wa Facebook jumbe zenye vitisho vya kigaidi mnamo tarehe nne mwezi huu, mashtaka ambayo ameyakana.

Mungai, ambaye pia ni mwanafunzi katika chuo kikuu cha Egerton, anadaiwa kuchapisha vitisho hivyo punde tu baada ya kutokea kwa shambulizi baya sana katika chuo kikuu cha Garissa.

Wanafunzi zaidi ya 143 waliuawa na wengine kuachwa na majereha mabaya ya risasi katika shambulizi hilo.

Swala la usalama limeleta joto sana nchini, na serikali inafanya kila jitihada ili kuzuia mashambuli ya kigaidi mfano wa lile la Garissa.